Serengeti Music Festival kuitikisa Dodoma

0
490

Historia itaandikwa kwa mara ya kwanza jijini Dodoma ambapo wasanii zaidi ya 70 wanatarajiwa kutoa burudani katika jukwaa moja la Serengeti Music Festival lililolandaliwa na serikali kwa lengo la kutangaza sekta ya utalii na kukuza sanaa.

“Serikali inafanya kazi kubwa sana hasa katika miradi mikubwa ya kimkakati, wakati miradi inatekelezwa kazi na dawa, tumeandaa tamasha kubwa barani Afrika pengine na duniani wasanii zaidi ya 70 wakubwa ku-paform katika jukwaa moja,” amesema Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt Hassan Abbasi

Amesema tamasha hilo kubwa litakalofanyika Februari 6, 2021 litaambatana na matukio mbalimbali kuanzia Februri 1, 2021 hadi kufikia siku ya kilele katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma.

FebruarI 4, 2020 kutakuwa na kongamano kubwa kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kwa mkoa wa Dodoma kukutana na watu maarufu hapa nchini katika nyanja za burudani na siasa kuwapitisha katika njia walizopita hadi kufika walipo sasa.

“Wanafunzi wa vyuo vikuu hapa Dodoma kukutana na role models wao katika sanaa na siasa watakuwepo watu maarufu watawapitisha njia walizopita hadi sasa wapo hivyo katika muziki, au siasa kila star ataeleza njia alizopita,” amesema.

Pia kutakuwa na mchezo wa mpira wa miguu kati ya madereva wa bajaj na Bodaboda, wabunge na wasanii wa Bongo flava na mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga kwa wanafunzi wa vyuo vikuu Dodoma.

“Tarehe 5 kutakuwa na Pre Party ambapo wasanii wakubwa watapaform ikiwa ni maandalizi ya kuelekea siku yenyewe ya tarehe 6 Jamhuri,” amesema Dkt. Abbasi

Ameongeza kuwa tamasha hilo litawapambanisha wasanii wa zamani ambao aidha waliacha muziki na kufanya kazi nyingine na makundi maarufu ya muziki ya zamani kama East Coast na TMK wanaume, sambamba na DJ maarufu wa zamani na wa sasa.