Rais Magufuli amsamehe Mkurugenzi Kahama

0
284

Akizungumza na Wananchi wa Shinyanga, Rais Dkt. John Magufu ametangaza kumsamehe Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Anderson Msumba, aliyekuwa anatuhumiwa kununua gari la kifahari kinyume na taratibu.

Mbali na kutangaza msamaha huo, Rais ameridhia mkurugenzi huyo aendelee kutumia gari hilo baada ya kuvutiwa na utendaji kazi wake mzuri katika miradi mitatu ambayo ameizindua leo.

“Niwaeleze ndugu zangu kwamba huyu mkurugenzi na madiwani wana akili sana, wametoa eneo bure hawakumuuzia yule muwekezaji, lengo lao wameangalia mbele zaidi kwamba kiwanda kitatengeneza ajira kwa wakazi wa eneo hili, kwa hiyo nimeamua kumsamehe mkurugenzi huyu, na hili gari namrudishia aendelee kuliendesha,” amesema Dkt. Rais Magufuli

Aidha, ameipongeza manispaa hiyo kwa kutenga fedha za miradi ambayo inagusa wananchi moja kwa moja wa eneo hilo ikiwemo ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na kupelekea kuongeza shilingi milioni 500 katika ujenzi wa jengo hilo.

“Kwa namna nilivyoona ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na jinsi uongozi wa hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kahama wanavyofanya kazi nzuri na usafi, basi naongeza milioni 500 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo hilo la OPD.”

Rais Dkt. Magufuli anatarajiwa kuendelea na ziara za uzinduzi wa miradi ya maendeleo ambapo Januari 29, 2021 atakuwa mkoani Tabora.