Majaliwa: Sitaki kusikia muwekezaji anacheleweshwa

0
439


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa serikali kutekeleza majukumu yao kwa wakati, waondoe urasimu kwani hataki kusikia mtu yeyote anayetaka kuwekeza nchini anakwamisha kutokana na utendaji wao.


Majaliwa ameongeza kuwa, serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuanzisha wizara maalum ya uwekezaji, kupambana na rushwa, kuimarisha upatikanaji wa ardhi, ujenzi na ukarabati wa miundombinu na kufuta tozo 173, ili kuhakikisha wawekezaji wanafanya kazi kwa ufanisi.

“Nia ya serikali ya awamu ya tano ni kuvutia wawekezaji, na wewe [mtumishi] ndiye facilitator [muwezeshaji],” amesema Majaliwa.

Akizundua Mwongozo wa Uwekezaji Mkoa wa Iringa amesema ni wazi kuwa uwekezaji wa aina yoyote unachochea upatikanaji wa ajira na kukuza matumizi ya teknolojia, hivyo watumishi wenye dhamana wasiwe vikwazo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kulia) akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi wakati wa uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji mkoani humo.


Amebainisha kuwa viashiria mbalimbali vinaonesha matunda ya jitihada za serikali ikiwa ni pamoja kukua kwa uchumi na kupungua kwa mfumuko wa bei ambao umefikia tarakimu moja.

Kiashiria kingine ni kuongezeka kwa mapato yanayokusanywa na serikali na kudhibiti matumizi yake kwa kuondoa shughuli zisizo na maslahi kwa umma.


Amefafanua kuwa Iringa ni sehemu bora zaidi ya kuwekeza kutokana na kuwa ardhi nzuri, uwepo wa maji ya kutosha, hali ya hewa ya kuvutia, uwepo wa nguvu kazi ya kutosha, barabara za lami.


“Mimi mwenyewe kuna siku nilipita kule Isimani, nikaona eneo nikalitamani, [Waziri] Lukuvi akaniambia hilo tayari,” amesema Majaliwa akieleza nia yake ya kuwekeza Iringa, mkoa alioubainisha kuwa ni eneo la kupumulia Makao Makuu ya Nchi, Dodoma.