Muuguzi aliyempiga vibao Mjamzito awajibishwa

0
172

Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania limemkuta na hatia Muuguzi Valentine Kinyanga wa kituo cha afya cha Mazwi kilichopo mkoani Rukwa, ambaye alidaiwa kumpiga vibao mama aliyefika kujifungua kituoni hapo tarehe 5 mwezi huu.

Akisoma hukumu hiyo mbele ya wakili wa Serikali Fortunatus Mwandu, Mwenyekiti wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania Abner Mathube amesema mlalamikiwa ametiwa hatiani chini ya kifungu 26(a)(c) ya sheria ya uuguzi na ukunga kwa kosa la kwanza na la pili.

Mathube amesema Baraza hilo lilichambua maelezo ya mlalamikiwa, mlalamikaji pamoja na mashahidi kuhusu kosa la kwanza la kumpiga mgonjwa kinyume na kifungu 25(3)(c) cha sheria ya uuguzi na ukunga Tanzania.

Katika kosa la kwanza, ushahidi umethibitisha ni kweli mlalamikiwa alimpiga mlalamikaji na mtuhumiwa amekiri kumpiga mlalamikaji.

Kosa la pili la kushindwa kusimamia maadili na weledi wa kitaaluma kinyume na kifungu 25(3)(k), imethibitika mtuhumiwa kushindwa kufuata utaratibu wa utoaji wa huduma za uuguzi na ukunga kwa mlalamikaji, kushindwa kuchukua na kuhifadhi taarifa za vipimo vya mgonjwa, kushindwa kufuatilia mwenendo wa uchungu wa mgonjwa wakati wa kumpokea katika kituo cha kutolea huduma na kuruhusu mtu ambaye sio mtaaluma kumpima mlalamikaji(mgonjwa).

Kutokana na ushahidi huo, Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania limefikia uamuzi wa kumuondoa Valentine Kinyanya kwenye orodha ya Wauguzi na Wakunga Tanzania na limemtaka arejeshe vyeti na leseni kwa Muuguzi mkuu wa mkoa wa Rukwa ambaye atawasilisha kwenye Baraza hilo.

Hata hivyo Baraza hilo limesisitiza kuwa Valentine ana haki ya kukata rufaa kwa Waziri Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ndani ya kipindi cha miezi mitatu tangu tarehe ya hukumu.