Mwongozo wa utoaji chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo wazinduliwa

0
151

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki amezindua mwongozo wa utoaji chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo nchini.

Mwongozo huo wenye lengo la kuhakikisha sekta binafsi na umma zinajua haki na wajibu katika zoezi zima la utoaji wa chanjo na kuhakikisha afya ya mnyama inabaki salama, umezinduliwa jijini Dodoma.
 
Waziri Ndaki amezindua mwongozo huo baada ya hivi karibuni kuagiza kusimamishwa kwa muda utoaji wa chanjo unaofanywa na halmashauri nchini kupitia kampuni walizoingia nazo mikataba, baada ya kubaini chanjo kutolewa kiholela kwa mifugo bila kuwepo utaratibu sahihi na kusababisha madhara kwa mifugo na hasara kwa mfugaji.
 
Katika kuhakikisha mwongozo wa utoaji wa chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo nchini unakuwa na tija kwa Taifa, Waziri Ndaki ametaka kuwepo kwa haki na wajibu kwa Wadau wote wa mifugo ili kuelewa vema haki na wajibu huo katika kusimamia mwongozo huo na kufikia matokeo chanya katika kuboresha afya ya mifugo.
 
“Mambo ya msingi kabisa kwenye jambo hili ni afya ya mifugo, afya ya mifugo ilikuwa hatarini, ni kweli utaratibu wanafanya halmashauri lakini hauko wazi sana, ndiyo maana tukasema sasa ni muhimu kuwa na mwongozo huu kutuelekeza nini cha kufanya, chanjo ikifanywa vizuri kwa usahihi bila makosa tuliyokuwa tunayaona tunaweza kuwa na ng’ombe wenye afya bora na njema,”amesema Waziri Ndaki.
 
Aidha, amesema mwongozo huo ambao umeshirikisha Wadau zaidi ya thelathini wakati wa kuuandaa, Wizara ya Mifugo na Uvuvi ipo tayari kupokea maoni ya Wadau sehemu ambazo utaonekana kuwa na mapungufu ili kuurekebisha na kuufanya uwe bora zaidi, lengo likiwa ni kuhakikisha afya ya mifugo nchini inalindwa na mfugaji kutopata hasara ya mifugo yake kufa au kupata madhara mengine yoyote baada ya kuchanjwa.
 
Katika kuhakikisha Serikali inaendeleza mahusiano mazuri na sekta binafsi, Waziri huyo wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki amesema wizara itahakikisha inaandaa mazingira mazuri ya kuwa pamoja na sekta binafsi ili kufanya kazi pamoja ambayo itakuwa na tija kwa Taifa na Wafugaji.
 
“Sekta binafsi nipende kuwahakikishieni kwamba sisi tutafanya kazi na sekta binafsi vizuri kabisa tusiwe na mashaka ni vile tuliona kasoro, lakini niwaombeni sekta binafsi hasa wale mlio vizuri katika jambo hili la chanjo msiwe na wasiwasi hata mkiingia mikataba na halmashauri ili mradi muwe na sifa na vigezo ndiyo maana ya sisi tukatoa mwongozo ili tufanye kazi pamoja,” amefafanua Waziri Ndaki.
 
Pia, amewataka viongozi wenzake wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, mamlaka za Serikali za Mitaa, watoa huduma za afya ya mifugo na sekretarieti za mikoa kuzingatia maelekezo yaliyopo kwenye mwongozo wa utoaji wa chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo nchini, na kutoa maoni au kuuliza maswali sehemu ambazo zitakuwa na utata ili kuhakikisha mwongozo huo unatekelezwa kama ambavyo umezingatiwa kwa ajili ya kudhibiti magonjwa ya mifugo nchini.
 
Amewaagiza Watendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutoa nakala za kutosha za mwongozo huo kwa Wadau wa sekta ya mifugo kote nchini, na pia kuwataka wadau kupata nakala laini kupitia tovuti ya wizara hiyo ambayo ni www.mifugouvuvi.go.tz.
 
Akimwakilisha mkuu wa mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge katika uzinduzi huo, mkuu wa wilaya ya Bahi Mwanahamisi Mukunda amesema kuwa, mkoa huo utahakikisha unayasimamia yale yote ambayo Wizara ya Mifugo na Uvuvi inatamani yafanyike katika sekta ya mifugo.