Ujenzi wa chuo cha mafunzo ya Uhamiaji washika kasi

0
218

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameelezea kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa chuo cha Mafunzo ya Uhamiaji cha Boma Kichakamiba kilichopo wilayani Mkinga mkoani Tanga.
 
Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akizungumza na Makamanda na Wadau mbalimbali mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa chuo hicho wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Tanga.
 
Ujenzi wa chuo hicho ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa  mwezi Oktoba mwaka 2020 akiwa wilayani humo, wakati akimnadi aliyekuwa mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt John Magufuli.


Waziri Mkuu amesema ujenzi wa chuo hicho ni jambo jema katika Idara ya Uhamiaji na kina manufaa makubwa nchini na kwamba ujenzi wa majengo hayo ni muendelezo wa jitihada za Serikali za kuhakikisha idara hiyo inafanya kazi kwa ufanisi.
 
“Katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya awamu ya tano, zipo jitihada kubwa zimefanywa za kuimarisha miundombinu kwenye majeshi yetu nchini, kwenye Idara ya Uhamiaji tumewezesha upatikanaji wa nyumba 103 za makazi pamoja na ujenzi wa jengo la makao makuu mkoani Dodoma,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.   
 
Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa  ameiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuhakikisha inatenga mapema bajeti kwa ajili ya Idara ya Uhamiaji ili  iweze kukamilisha miundombinu ya chuo hicho.
 
Waziri Mkuu pia ameipongeza Idara ya Uhamiaji kwa namna inavyofanya kazi kwa weledi na kuibua mbinu mbalimbali zinazotumiwa na Wahamiaji wanaoingia nchini bila kufuata utaratibu.
 
Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt Anna Makakala amesema lengo la kuanzishwa kwa chuo hicho cha Mafunzo ya Uhamiaji cha Boma Kichakamiba ni kutoa mafunzo ya utayari kwa wakati na gharama nafuu, kupata askari wenye ukakamavu, nidhamu, weledi na maadili ya kikazi ya kiuhamiaji.
 
Dkt Makakala amesema kuwa mpaka sasa zimetumika shilingi milioni 140 katika ujenzi huo, fedha zilizotokana na michango ya hiari ya maafisa na askari wa uhamiaji waliochangia shilingi milioni 81 huku wadau wengine wakichangia shilingi milioni 59.