Joto lapanda kuelekea tamasha la Wasafi Media Tumewasha na Tigo

0
348

Kuelekea Tamasha la Wasafi Media Tumewasha na Tigo litakalofanyika jijini Dar es salaam, Afisa Mtenfaji Mkuu wa kampuni ya Wasafi Media Msanii Naseeb Abdul maarufu kwa jina la Diamond Platinumz, amesema tamasha hilo litafanyika pamoja na utoaji wa huduma za kijamii kwa Wananchi.

Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Diamond amesema ili kufanikisha tamasha hilo kwa ubora unaotakiwa, wamejipanga kutoa huduma ya upimaji wa afya bure kwa Wananchi wote.

“Ili burudani iweze kufana tumeona tutoe huduma za upimaji wa afya bure kwa Wananchi wote kabla ya kufanya tamasha kwa ajili ya usalama wao,”amesema Diamond.

Ameongeza kuwa katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha sekta ya elimu nchini, kampuni ya Wasafi Media kwa kushirikiana na wadau wengine wa elimu watachangia madawati elfu moja yatakayotumiwa na shule mbalimbali zenye upungufu wa madawati jijini Dar es salaam.

“Tunatambua kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya awamu ya tano katika utoaji wa elimu bila malipo kwa watoto wa Kitanzania, hivyo tumeona tutumie pia fursa hii kuchangia madawati elfu moja kupunguza pengo la uhitaji wa madawati katika shule zetu, ” amesisitiza Diamond.

Kuhusu Wasanii watakaotumbuiza katika tamasha hilo la Wasafi Media Tumewasha na Tigo, Diamond amesema kuwa ni vema Wasanii wote wakawa wamejisajili Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza wakati wa tamasha hilo.

“Hatutaruhusu Msanii yeyote ambaye hajasajiliwa na BASATA kupanda jukwaani kutumbuiza, tuheshimu sheria na taratibu zilizowekwa maana hatutaki tena kuharibu shughuli yetu na nyie wenyewe mnafahamu tumefungiwa matangazo ya TV hivyo hatukubali kufungiwa tena na redio, ” amesema Diamond.

Tamasha la Wasafi Media Tumewasha na Tigo linatarajiwa kufanyika tarehe 30 mwezi huu katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam, likitanguliwa na michezo mbalimbili ikiwa ni pamoja na mpira wa miguu utakaowakutanisha Wasanii na Watangazaji.