Wakazi wa Ifakara wafurahia huduma katika hospitali ya rufaa ya Mt Fransisko

0
209

Wakazi wa Ifakara mkoani Morogoro wameishukuru Serikali kwa namna inavyoshirikiana na
Hospital ya Rufaa ya Mtakatifu Fransisko kuwapatia huduma mbalimbali za kitabibu.

Wakazi hao wametoa shukrani zao wakati wa uzinduzi wa majengo ya upasuaji, maabara na vifaa vya kisasa vilivyofadhiliwa na Serikali ya Uswisi.

“Nimeleta mgonjwa wangu hapa, nimeona anavyohudumiwa vizuri na nipongeze juhudi zinazofanywa za kuboresha huduma hapa hospitalini,” amesema Esta Komba mkazi wa Ifakara.

Askofu wa Katoliki Jimbo la Ifakara Salutaris Libena amesema hospitali hiyo ilikuwepo tangu enzi ya mkoloni na kwa ushirikiano wa Serikali za Tanzania na Uswisi iliweza kuendelea kutoa huduma katika ngazi mbalimbali hadi kufikia kuwa Hospitali ya Rufaa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa yasiyoambukiza wa hospitali hiyo ya Rufaa ya Mtakatifu Fransisko Dkt James Charles amesema, hospitali hiyo ina umuhimu kwa wakazi wa mkoa wa Morogoro, hivyo wataendelea kutoa huduma kwa kiwango kinachotakiwa.

“Serikali ya awamu ya tano inajipambanua katika kuboresha maisha ya Watanzania ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za afya, ndio maana kwa kushirikiana na wadau mbalimbali tunazidi kuboresha huduma hizo kila siku,” ameeleza Dkt Charles.

Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Fransisko ni moja ya hospitali kongwe hapa nchini iliyoanzishwa tangu enzi ya ukoloni, na baadae Serikali ikaikabidhi kwa Kanisa la Katoliki kwa ajili ya kuiendeleza.

Kwa muda mrefu sasa, Serikali ya Uswisi kwa kushirikiana na Wadau wengine wa afya wamekuwa wakichangia nguvu zao, lengo likiwa ni kuboresha mazingira pamoja na huduma mbalimbali zinazotolewa.