Madiwani watatu Mbinga mikononi mwa TAKUKURU

0
166

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Ruvuma, Hamza Mwenda ahakikishe anawakamata Madiwani na Watendaji wa halmashauri ya Mbinga Vijijini ili wajibu tuhuma za rushwa zinazowakabili.
 
Madiwani hao ni wa kata za Mkumbi, -Bruno Kapinga, kata ya Lukalasi, – Bosco Ndimbo na wa kata ya Linda ambao wanadaiwa kuchukua fedha kutoka kwa Watendaji wa AMCOS kwa ajili ya kwenda kushawishi kuhamishwa kwa eneo la ujenzi wa makao makuu ya halmashauri hiyo.
 
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo baada ya kuzindua jengo la utawala la halmashauri ya mji wa Mbinga akiwa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma.

Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa mkoa wa Ruvuma,- Christine Mndeme asimamie ujenzi wa halmashauri hiyo unaoendelea katika eneo la Kigonsera.
 
Hatua hiyo imekuja baada ya kuwepo kwa mvutano wa Madiwani wa halmashauri ya Mbinga Vijijini ambao baadhi yao hawataki makao makuu ya halmashauri hiyo yajengwe Kigonsera na kuamua kuendesha mchakato wa kushawishi wengine wagomee mradi huo, jambo ambalo linakwamisha maendeleo kwa sababu tayari mradi huo umeshaanza kujengwa.
 
Mvutano huo unaongozwa na Madiwani wa Kata tatu za Mkumbi, Lukalasi na Linda ambao wanataka makao makuu yajengwe kwenye kata ya Mkumbi katika eneo ambalo litailazimu Serikali ilipe fidia ya zaidi ya shilingi milioni 400 huku kukiwa na eneo la bure la ekari 150 ambalo ndiko yanakojengwa makao makuu.
 
“Hatuwezi kukubali huko mnakotaka nyie ni lazima tulipe fidia ya zaidi ya shilingi milioni 400 na kuna eneo la bure ekari zaidi ya 150, hii haikubaliki hatuwezi kufanya mambo ya siasa kwenye fedha za Wananchi haiwezekani, mmeamua kila AMCOS ichange shilingi 600,000 mpate milioni tatu mfanye kampeni ya kutaka halmashauri ijengwe kweni hiyo ni rushwa,”amesema Waziri Mkuu Majaliwa.