Marufuku Wafanyabiashara kuchanja mifugo : Waziri Ndaki

0
173

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki amepiga marufuku halmashauri zote nchini kutumia Wafanyabiashara kuchanja mifugo, na kutaka kuvunjwa kwa mikataba hiyo mara moja.

Waziri Ndaki amebainisha hayo mkoani Shinyanga alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja, ambapo alipokuwa katika josho la kuogeshea mifugo la kijiji cha Mipa kilichopo wilayani Kishapu kwa ajili ya kushuhudia uogeshaji mifugo na utoaji wa chanjo ya homa ya mapafu kwa ng’ombe, Wafugaji wamemlalamikia kuwa baadhi ya ng’ombe kijijini hapo wamekuwa wakivimba na wengine kufa baada ya kupatiwa chanjo.

Waziri Ndaki akiwa ameongozana na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Pauline Gekul amesema kuwa, kuanzia sasa chanjo zote nchini zitatolewa na Wataalamu wa wizara ambao wamethibitishwa na kugoma kushuhudia zoezi la uchanjaji lililokuwa limeandaliwa baada ya kukasirishwa na uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu kutokuwa na takwimu yoyote ya idadi ya ng’ombe waliovimba na wengine kufa baada ya kuchanjwa.

“Halmashauri zetu zote kuanzia sasa hivi ni marufuku kutumia Wafanyabiashara kuchanja mifugo yetu, halmashauri zitumie Wataalamu wa wizara ambao wamethibitishwa waweze kuchanja mifugo ya Wananchi wetu, hao Wafanyabiashara kama mmeingia mikataba nao hiyo mikataba ivunjeni haraka iwezekanavyo hatuwezi kuchezea akili za watu namna hii hatuwezi kutuma Wafanyabiashara waende kuchanja ng’ombe wanavimba na wanakufa halafu taarifa hatuna,” ameagiza Waziri Ndaki.

Akiwa katika ziara yake hiyo ya siku moja mkoani Shinyanga, Waziri Ndaki amefika katika mnada wa upili wa Mhunze ambao ni moja ya minada inayosimamiwa na wizara ya Mifugo na Uvuvi na kumuagiza Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu kumuondoa mara moja kazini Mhasibu wa halmashauri hiyo anayefanya kazi katika mnada huo Athanas Msiba, kwa tuhuma za kutokuwa mwaminifu katika kuandika idadi ya mifugo inayoingia na kutoka katika mnada huo, hali inayosababisha wizara na halmashauri kukosa mapato stahiki.

“Mkurugenzi huyu Athanas Msiba siyo mwaminifu, hafai kukaa hapa tena aondoke sasa hivi ulete mtu mwingine, watu wakipita hapa na mbuzi watano anaandika watatu anaandika kidogo hafai aondoke hapa,” amesema Waziri Ndaki.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu, – Emmanuel Johnson amesema amepokea maelekezo hayo na atayafanyia kazi kwa kuihusisha pia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU), ili ifanye ufuatiliaji kwa kuwa Serikali haiko tayari kuwa na watu wenye tabia ya namna hiyo.

Waziri Ndaki pia amepata fursa ya kusikiliza kero mbalimbali kutoka kwa Wafanyabiashara na Wafugaji waliokuwepo mnadani hapo ikiwemo ile ya kuzuiwa kuondoa mifugo mnadani kabla ya saa 12 jioni, hali inayohatarisha maisha yao kutokana na uwepo wa fisi wengi kwenye maeneo ya mashamba wakati wa kurudi nyumbani majira ya jioni.

Akijibu kero hiyo, Waziri Ndaki ameuagiza uongozi wa mnada huo wa upili wa Mhunze, utafute utaratibu wa kuwaruhusu Wafanyabiashara kuondoka kabla ya muda huo wakiwa wamemaliza shughuli zao.

“Mtu amemaliza biashara yake mkagueni vizuri kwenye mlango wa kutokea aende zake akimaliza hapa akikaa saa mbili aondoke, akikaa dakika 15 aondoke ili mradi amemaliza shughuli zake siyo unawaleta unawafungia humu haka kamekuwa kajela kadogo?, hapana hiyo,” amesisitiza Waziri huyo wa Mifugo na Uvuvi.