Mgodi wa Nyangalata kupata umeme

0
150

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani ameendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Shinyanga, kwa kutembelea mgodi mdogo wa uchimbaji madini ya dhahabu wa Nyangalata uliopo katika halmashauri ya Msalala wilayani Kahama.

Akiwa katika mgodi huo akifuatana na Mbunge wa jimbo la Msalala, -Iddi Kasimu, Mkuu wa wilaya ya Kahama,- Anamringi Macha, pamoja na maofisa kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dkt Kalemani amesema Serikali inataka kasi ya usambazaji umeme kwenye migodi midogo ya madini ili kuondoa gharama kubwa za uzalishaji wa madini hayo.

Amesema migodi midogo ya uchimbaji wa madini ya dhahabu imekuwa ikitumia gharama kubwa ya uzalishaji wa madini hayo kutokana na kutumia mafuta mazito ama Jenereta, lakini wakitumia Nishati ya umeme kutoka Gridi ya Taifa hawatakuwa wakiingia kwenye gharama hizo kubwa kama ilivyo sasa.

“Rais John Magufuli ameshatoa fedha ili Wananchi wasambaziwe huduma ya umeme yakiwamo na maeneo ya migodi midogo, hivyo naagiza Januari 3 mwaka 2021, watu wa Survey wawe wameshafika kwenye eneo hili la mgodi wa Nyangalata na kuanza mchakato wa kuleta huduma ya umeme hapa, pamoja na kwenye mgodi wa Tambarare,” amesema Dkt Kalemani.

Pia amesema kuwa, hadi kufikia Februari 5 mwaka 2021, Serikali inatarajia kuanza kusambaza huduma ya nishati ya umeme kwenye vitongoji na vijiji vyote nchi nzima, ambapo katika wilaya ya Kahama vimesalia vijiji 147, na halmashauri ya Msalala kuna vijiji 60.

Kwa upande wake mmoja wa wachimbaji wadogo wa dhahabu katika mgodi huo wa Nyangalata, – Alex Manyama amesema kutokana na kutumia mafuta mazito kuzalisha madini ya dhahabu, amekuwa akitumia Shilingi Laki Tisa kwa siku na hivyo kuiomba na Serikali iwapelekee huduma hiyo ya Nishati ya umeme ili kuwapunguzia matumizi hayo makubwa.