Serikali kuwawezesha Vijana wabunifu kwenye TEHAMA

0
137

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt Faustine Ndugulile amesema kuwa, Serikali itaweka mazingira wezeshi ya kuendeleza vijana wabunifu wa TEHAMA.

Dkt Ndugulile ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati wa ziara yake ya kutembelea Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na Ndaki ya TEHAMA ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (COICT).

Amesema Vijana wanabuni mifumo mbalimbali ya TEHAMA ya kutatua changamoto za Wananchi, ila wanakosa mazingira wezeshi ya kuendeleza na kukuza bunifu zao, kama vile kupatiwa muda maalumu wa kuingiza sokoni bunifu zao kwa kufanya majaribio ya bunifu hizo kukubalika kwa Wananchi bila kulazimika kulipia gharama za usajili, kupata masoko, malipo ya kodi na leseni kuendana na matakwa ya uendeshaji wa kampuni na biashara nchini.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH Dkt Amos Nungu amesema kuwa, Vijana hao wameanzisha kampuni zaidi ya 20 za mifumo ya TEHAMA, na tayari mifumo hiyo inasaidia kukusanya kodi kwenye halmashauri; kuwawezesha vijana kusoma VETA kwa njia ya mtandao na kampuni ya simu za mkononi ya TIGO kuweza kuhifadhi taarifa za Wateja wake.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu, Utafiti na Ubunifu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam Profesa Benadetha Kiliani na Mkuu wa Ndaki ya TEHAMA ya Chuo hicho Dkt Mussa Kisaka wamesema kuwa Chuo kiko tayari kushirikiana na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ili kuendeleza Vijana wabunifu na watafiti wa TEHAMA nchini.

Akizungumza kwa niaba ya Vijana wabunifu wa TEHAMA, Geofrey Magila ameiomba Serikali kuwawezesha wakubalike na kuaminika na wapewe kazi badala ya kampuni zao kufanya kazi kwa kutumia mgongo na majina ya kampuni nyingine kwa kuwa kampuni zao ni changa na hazina mtaji wa kutosha kuingia kwenye ushindani wa zabuni zinazotangazwa zinazohusu mifumo ya TEHAMA.