Askofu Banzi azikwa Tanga

0
179

Waziri MKuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania kumuenzi Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Tanga, Anthony Banzi kwa kuuishi utumishi wake uliotawaliwa na upole na unyenyekevu.
 
Waziri Mkuu ametoa wito huo mkoani Tanga wakati wa mazishi ya Askofu Banzi yaliyofanyika ndani ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Anthony wa Padua, Jimbo Katoliki la Tanga.

Amesema wakati wa uhai wake, Askofu Banzi alitoa mchango mkubwa katika sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na elimu, afya na maji.

“Leo hii tunapomsindikiza Baba Askofu Anthony Banzi tunajivunia mchango wake mkubwa katika kupigania amani, maelewano na mtangamano wa jamii kwa lengo la kujenga umoja, upendo na mshikamano wa Kitanzania, Sisi upande wa Serikali tutamkumbuka sana.” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Waziri Mkuu Majaliwa ameshiriki mazishi hayo kwa niaba ya Rais Dkt John Magufuli.

Askofu Banzi alifariki dunia Jumapili Desemba 20 katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.