Serikali kuendelea kuthamini mchango wa Viongozi wa dini

0
333

Serikali imesema itaendelea kuthamini mchango wa Viongozi wa dini katika maendeleo ya Taifa, na inathamini dua na maombi yao hasa wakati wa kipindi cha ugonjwa wa Corona.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo, wakati wa kufunga shindano la kusoma Qur’aan kwa Wazee wa Kiislamu wa mkoa wa Dar es salaam, tukio lililofanyika pamoja na ufunguzi rasmi wa mashindano ya 21 ya kusoma Qur’aan Barani Afrika.

“Tumeshuhudia Taifa letu na dunia nzima ikipita katika changamoto ya ugonjwa wa Corona, lakini kutokana na Imani thabiti ya Rais wetu na Viongozi wa dini kwa Mwenyezi Mungu Taifa limeweza kuvuka salama katika changamoto hiyo,”amesema Waziri Jafo.

Ameongeza kuwa mashindano ya Qur’aan ‘yamekuwa msaada mkubwa katika kulitangaza Taifa la Tanzania duniani, hivyo kuwataka Viongozi hao kuendelea kuboresha mashindano hayo kama sehemu ya kupaisha Utalii wa nchi duniani.

Katika uzinduzi huo, Waziri Jafo ameipongeza Taasisi ya Al-Hikima kwa kuandaa mashindano ya kusoma Qur’aan Tukufu kwa Wazee wa mkoa wa Dar es salaam na kubainisha kuwa hatua hiyo itaongeza ari ya vizazi vijavyo kuhifadhi Qur’aan Tukufu.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Al-Hikima Foundation Sheikh Nurdeen Kishk amesema kuwa taasisi hiyo inajivunia uongozi wa Rais Dkt John Magufuli kwa namna anavyosimamia haki ya kuabudu kwa dini zote nchini.

“Kama Waislamu hatuna budi kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Rais Dkt John Magufuli kwa kusimamia imani ya Mwenyezi Mungu kwa dini zote nchini, tumeshuhudia mengi kipindi cha miaka mitano iliyopita ya uongozi wake hasa katika matukio makubwa ya Kitaifa yanayoandaliwa na Viongozi wa dini,” amesema Sheik Kishk.

Aidha amebainisha kuwa lengo la kuwashindanisha Wazee wa mkoa wa Dar es salaam kabla ya mashindano makuu Barani Afrika ni kuleta hamasa kwa Wanafamilia kujijengea utamaduni wa kuhifadhi Qur’aan Tukufu kwa manufaa ya maisha yao ya kila siku.

Mshindi wa kwanza katika shindano hilo kwa Wazee wa mkoa wa Dar es salaam ambalo liliwashindanisha Wazee arobaini, amejinyakulia kitita cha shilingi milioni moja huku mshindi wa pili akiondoka na shilingi laki nane.

Mashindano makubwa ya 21 ya kusoma Qur’aan Tukufu Barani Afrika yanatarajiwa kufanyika mwezi Mei mwaka 2021, ambapo zaidi ya nchi thelathini zinatarajiwa kushiriki.