Serengeti Boys kumenyana na Uganda fainali CECAFA

0
292

Kikosi cha timu ya Taifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 (Serengeti Boys), leo kinashuka dimbani kumenyana na vijana wa Uganda katika mchezo wa fainali ya michuano ya CECAFA.

Serengeti boys imefuzu kucheza fainali baada ya ushindi wa penati 4-3 dhidi ya Ethiopia kufuatia sare ya bao 1-1 kwenye mchezo wa nusu fainali uliochezwa kwenye uwanja wa Umuganda mjini Rubavu, nchini Rwanda.

Licha ya kumenyana na katika mchezo huo wa fainali, tayari timu zote mbili za Serengeti Boys na The Cobs zimefuzu kucheza  fainali za AFCON kwa vijana hao wenye umri wa chini ya miaka17 zitakazofanyika mwezi julai mwaka 2021 nchini Morocco.

Hii inakuwa mara ya tatu mfululizo kwa Serengeti Boys kufuzu kucheza fainali za AFCON, wakifanya hivyo mwaka 2017 katika fainali zilizofanyika nchini Gabon na 2019 zilipofanyika nchini Tanzania.

Serengeti Boys, ambao ni mabingwa wa CECAFA u-17 mwaka 2018, wanafuata nyayo za kaka zao Ngorongoro Heroes waliofuzu fainali za AFCON kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 20, fainali zitakazofanyika nchini Mauritania kuanzia Februari 14 hadi Machi 4 mwaka 2021.