Mawakala wanaotoa huduma za bima watakiwa kufika vijijini

0
184

Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA)
Dkt Mussa Juma amesema sekta ya bima ina mchango mkubwa katika kulinda mali na afya za Watanzania, hivyo mawakala wanaotoa huduma hiyo wanapaswa kuhakikisha huduma hiyo inawafikia Watanzania wengi zaidi hasa wa maeneo ya vijijini.

Akizungumza jijini Dar es salaam mara baada ya kufungua mkutano wa mwaka wa Mawakala wa Bima nchini, Dkt Juma amesema kila Mtanzania anapaswa kuona umuhimu wa kuwa na bima ili kulinda afya na mali zake.

“Ukiwa na bima utakuwa umejihakikishia huduma bora za afya na ulinzi wa mali zako na za familia yako, lakini pia utakuwa umelipunguzia Taifa gharama kubwa ya kukuhudumia,” amesisitiza Kamishna huyo wa TIRA.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mawakala wa Bima Tanzania Bara Sayi Daudi amezungumzia umuhimu wa wananchi kuwa na bima ya ajali na kusema kuwa hatua hiyo itakuwa msaada mkubwa pindi wanapopata ajali za aina mbalimbali.

“Wapo watu wengi wanapata ajali za pikipiki na vyombo vingine vya usafiri na kusababisha ulemavu kwa baadhi yao, hivyo kuwa na bima itakayokuhudumia wakati wa majanga kama hayo kutakuhakikishia huduma ya afya wakati wowote ule,” amesema Sayi.

Nao baadhi wa washiriki wa mkutano huo akiwemo Mwenyekiti wa Bima Visiwani Zanzibar, – Issa Twahir Omar na Aneth Mwakagali wamewataka Wananchi kuwaepuka Mawakala wa Bima wanaotoa huduma kinyume na taratibu, ambao wamekuwa wakitoa bima zisizotambuliwa na taasisi mbalimbali za Serikali.