Waliohusika na ununuzi wa magari ya kifahari wapewa siku 7 kujieleza

0
202

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa muda wa siku Saba kwa Wakurugenzi Watendaji wa halmashauri nne nchini kujieleza walikotoa fedha na mamlaka ya kununua magari ya gharama kubwa kwa ajili ya kutembelea.

Akizungumza jijini Mwanza na Watumishi wa umma, Wabunge, Madiwani wa jiji la Mwanza na Manispaa za Ilemela na Nyamagana, Waziri Mkuu amewataja Wakurugenzi hao kuwa ni wale wa halmashauri ya Jiji la Mwanza, Msalala, Kahama na Chato mkoani Geita.

Pia ametoa muda huohuo wa siku Saba kuanzia leo, kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu na Maofisa wanaochambua maombi ya ununuzi wa magari Ofisi ya Waziri Mkuu nao wajieleze ni kwa nini magari katika halmashauri hizo yalinunuliwa kwa gharama kubwa.
 
Amesema ununuzi wa magari hayo ni matumizi mabaya ya fedha za umma na haiwezekani viongozi hao watumie magari ya gharama kubwa badala ya kutumia fedha hizo kwa ajili ya maendeleo ya wananchi, na ametaka muongozo wa ununuzi wa magari uliotolewa na Serikali uzingatiwe.
 
Waziri Mkuu Majaliwa amesisitiza matumizi ya fedha za umma lazima yasimamiwe ipasavyo na kwamba Serikali haina mzaha na mtumishi yeyote atakayebainika kutumia vibaya fedha za umma.