Mawakala wanaoficha saruji waonywa

0
216

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza wizara ya Viwanda na Biashara ikamilishe utaratibu wa kuwa na bei kikomo ya saruji ili kuuwezesha kila mkoa kujua bidhaa hiyo inapaswa kuuzwa kwa bei gani, lengo likiwa ni kuondoa upandishwaji holela unaofanywa na wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo  jijini Dodoma, wakati wa mkutano wake na Wakuu wa mikoa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia uchukuzi, Maafisa Biashara wa mikoa, Mawakala wa saruji walioko mikoani na Wakurugenzi wa viwanda vya saruji, mkutano uliofanyika kwa njia ya Video.

Pia amewataka mawakala wa saruji kutoficha bidhaa hiyo kwa lengo la kupandisha bei kwa sababu kitendo hicho ni sawa na uhujumu uchumi na kwamba watakaobainika kufanya hivyo watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.

 “Mawakala badilikeni na acheni tabia ya kuficha bidhaa kwa ajili ya kuzipandisha bei, ukikutwa unatengeneza mazingira ya kuifanya bidhaa isipatikane kwa lengo la kuipandisha bei huo ni uhujumu uchumi, ukikamatwa na bidhaa ambayo inatafutwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yako”, ameonya Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema lazima utaratibu wa kuwa na bei kikomo ya saruji ukamilike ili kujua kila mkoa bidhaa hiyo inapatikana kwa kiasi gani.

“Mfano saruji inazalishwa Tanga au Dar es Salaam alafu Morogoro inauzwa kwa shilingi 28,000 sasa Kigoma itauzwaje lazima kuwe na bei kikomo”, amesisitiza Waziri Mkuu.

 Waziri Mkuu Majaliwa ametumia mkutano huo kuiagiza Tume ya Ushindani (FCC)  kufanya ukaguzi ili kubaini kama bei za saruji ni shindani na zina tija kwa wananchi kwa sababu katika maeneo mengine nchini  hazina uhalisia na zinasababisha usumbufu.
 
Amewaagiza viongozi wa Wizara ya Viwanda na Biashara kutembelea viwanda mbalimbali vya saruji  ili kusikiliza matatizo yanayovikabili na kushirikiana navyo ili kuyapatia ufumbuzi matatizo hayo.