Ujenzi wa SGR Morogoro – Dodoma wafikia asilimia 48

0
301

Awamu ya pili ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kuanzia Morogoro hadi Dodoma umefikia takribani 48%, huku shughuli za ujenzi zikiendelea kwa kasi.

Hayo yamesemwa na mhandisi msaidizi wa mradi kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC), Christopher Mangwe’la wakati akitoa maelezo kwa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo waliotembelea mradi huo wa kimkakati.

Mhandisi Mangw’ela ameongeza kuwa mradi huo una jumuisha vivuko takribani 110 pamoja na madaraja takribani 160 na kuongezo kuwa “Reli hii itakua na uwezo wa kutembea kilometa takribani 160 kwa saa na ina mahandaki manne ambayo mawili kati ya hayo yana urefu wa mita zaidi ya 800.”

Kwa upande wake mkuu wa msafara ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango, Petro Lyatuu amesema kwamba ziara hiyo imekuwa na manufaa kwa kuwa wajumbe wa baraza wamejifunza kwa vitendo namna mradi unavyotekelezwa hatua kwa hatua.

“Tumekua na siku nzuri leo tumejifunza kwa kuona jinsi Serikali inavyotekeleza mradi huu, tumeona hatua iliyofikiwa katika ujenzi ikiwemo usimikwaji wa nguzo za umeme pamoja na utandikaji wa mataruma ya reli, naamini tutakua mabalozi wazuri katika kuelimisha na kushawishi wengine waje wajifunze na kuona kazi inayofanyika hapa” amesema Lyatuu.

Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) unasimamiwa na Kampuni ya Reli Tanzania (TRC) huku mkandarasi akiwa ni Kampuni ya Yapi Merkezi pamoja na Korea Railroad Corporation (Korail) na unatarajiwa kukamilika mwaka 2021 kwa gharama ya takriban Shilingi trilioni 7.