Walimu kizimbani kwa kuvujisha mitihani

0
346

Walimu watano wa shule ya msingi Siashimbwe, wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi mkoani Kilimanjaro kwa makosa manne ikiwemo kosa la kuvujisha mitihani ya darasa la Saba ya masomo ya Kiswahili na Hisabati.

Waliofikishwa mahakamani ni Phillip Akonay, Fredrick Lyatuu, Flora Elias, Elionera Shirima na Eutika Tesha ambapo kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka mawili ikiwemo kushindwa kutunza karatasi za mtihani wa darasa la saba.

Akisoma mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mwandamizi wa wilaya, Naomi Mwerinde, wakili wa serikali Nitike Emmanuel, amesema mnamo Oktoba 7 mwaka huu katika Shule ya Msingi Siashimbwe iliyopo wilayani Moshi kwa pamoja washitakiwa walitoa mtihani wa darasa la saba wa somo la Hesabu katika chumba cha mtihani hali ya kuwa ni kinyume cha sheria.

Wakili Nitike amesema kitendo cha kushindwa kutunza karatasi za mitihani ya darasa la saba, ni kinyume na kifungu cha sheria namba 20 kifungu kidogo cha kwanza na sheria namba 24 kifungu cha 1 cha sheria ya baraza la Mitihani sura namba 107 marejeo ya mwaka 2009.

Amesema mtuhumiwa wa kwanza Phillip Akonay, anakabiliwa na na mashtaka mengine mawili ikiwemo kukutwa na karatasi ya majibu ya mtihani wa darasa la saba somo la Kiswahili huku akitambua kuwa ni kosa na kinyume cha sheria.

Akitoa masharti ya dhamana Hakimu Mwandamizi Naomi, amesema dhamana ipo wazi ambapo kila mshatakiwa anatakiwa kuweka dhamana ya bodni ya Milioni moja kila mmoja pamoja na kuwa na wadhamini wawili.

Hata hivyo washtakiwa hao wameshindwa kukidhi vigezo vya dhamana hivyo wamerudishwa rumande ambapo kesi hiyo itatatajwa tena Disemba 11 mwaka huu.