Halima Aden: Aacha mitindo kuisimamia imani yake

0
305

Mwanamitindo Halima Aden maarufu kama mlimbwende wa Hijabu, ametangaza kuachana na kazi hiyo, kwani imemfanya kuwa mbali na imani yake.

Aden (23) alijizolea umaarufu mwaka 2016 alipokuwa akishindana katika mashindano ya Miss Minnesota akiwa na miaka 18 na kuendelea kuwa mwanamitindo wa kampuni mbalimbali kubwa ikiwemo IGM, Fenty ya Rihanna na kampuni ya Kanye West, Yeezy.

Mwanadada huyo ambaye amevunja rekodi na kuwa mwanamitindo wa kwanza kuvaa hijabu kwenye majarida makubwa kama British Vogue, Allure na Vogue Arabia ameeleza kuwa moja kati ya sababu za kukaa mbali na kazi hiyo ni pamoja na kupoteza ukaribu na imani yake.

Ameeleza kuwa kazi yake ilimfanya akawa anakosa kusali kwa wakati kama anavyopaswa kulingana na imani ya dini yake ya Kiislamu na kukubali kazi ambazo zilimlazimu kutokuvaa hijabu na badala yake kujifunika kichwa na vitalba au nguo tofauti na hijabu.

Katika mtandao wake wa Instagram ameeleza sababu za kufikia uamuzi huo, pia ameonesha baadhi ya kazi ambazo alizifanya na hapendezwi nazo kwani hazimtambulishi yeye.

Aidha, kupitia video yake aliyoiweka Instagram, mama yake ameelezea kutopendezwa na kazi hiyo anayofanya mwanae.

Aden mwenye uraia wa Somalia-Marekani alizaliwa katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma, Kenya kwa wazazi wenye asili ya Kisomali na hapo baadaye kuhamia Marekani.