Spika wa Bunge Job Ndugai, amewaapisha wabunge wa 19 wa Viti Maalumu wanaotokana na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo-CHADEMA hii leo kwenye Viwanja vya Bunge Jijini Dodoma.
Miongoni mwa wabunge wa Viti maalumu walioapishwa ni pamoja na waliowahi kuwa wabunge kupitia chama hicho katika Bunge la 11.
Wabunge hao ni Pamoja na Halima Mdee (Aliyekuwa Mbunge wa Kawe), Esther Matiko (Aliyekuwa Mbunge wa Tarime Mjini), Ester Bulaya (Aliyekuwa Mbunge wa Bunda Mjini), Anantropia Theonest, Jesca Kishoa na Grace Tendega.
Akizungumza kwa niaba ya wabunge wa Viti maalum wa CHADEMA walioapishwa hii leo na Spika, Halima Mdee amesema watawatumikia wananchi kwa nguvu zote ili kuhakikisha wanapata maendeleo.
“Nikuhakikishie mheshimiwa spika tutafanya kazi kwa uaminifu kama kambi rasmi ya upinzani bungeni na kwa uadilifu mkubwa kwa viwango vilevile tulivyokuwa tunavifanya. Kuna vijana wapya sisi kama dada zao tunakuhakikishia watafanya kazi bora. Niwahakikishie wana Chadema tutafanya kazi mliyotutuma kwa uaminifu na uadilifu mkubwa sana.”Amesema Halima
Kwa upande wake Spika wa Bunge Job Ndugai amesema atawapa ushirikiano mkubwa wabunge hao ili waweze kutekeleza vyema majukumu yao ya kuwatumikia wananchi wakiwa Bungeni.
“kwanza niwapongeze kwa kula kiapo na kuwa wabunge katika Bunge la 12, lakini pia niwaahidi mimi kama spika nitawapa ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yenu licha ya uchache wenu” Amesema Spika Ndugai.