Serikali ya Ethiopia yaimarisha ulinzi jimbo la Tigray.

0
508

Serikali nchini Ethipia imepeleka wanajeshi zaidi katika jimbo la Tigray nchini humo kwa madai ya kuimarisha ulinzi wa amani katika jimbo hilo licha ya baadhi ya jumuiya za kimataifa kutaka kufanyika kwa mazungumzo ili  kumaliza mapigano kati ya vikosi vya serikali na wapiganaji wa jimbo hilo la Tigray.

Mapema hii leo vikosi vya serikali ya Ethipoa vimetumia njia ya barabara kuelekea katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Tigray ambapo taarifa za serikali ya nchi hiyo zikisema hatua hiyo ina lengo la kuongeza juhudi za kusimamia utii wa sheria na kukabiliana na baadhi ya wapiganaji waoendesha vitendo vya uvunjifu wa sheria.

Hata hivyo uongozi wa kisiasa katika jimbo hilo la Tigray umetoa wito kwa umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kuingilia kati mgogoro huo na kutafuta suluhu kwa kufanya mazungunzo ya amani.

Tayari rais Yoweri Museveni wa Uganda amekutana na kufanya mazungumzo na baadhi ya mawaziri wa serikali ya Ethiopia ili kutafuta suluhu ya mgogoro unaendelea ambapo rais wa zamani wa Nigeria  Olusegun Obasanjo ameripotiwa kuelekea nchini Ethiopia kuanzisha juhudi za kufanyika kwa mazungumzo ya amani kutatua mgogoro huo.

Kwa upande wake waziri wa mambo ya nje wa Ethiopia Redwan Hussein amesema serikali nchini humo haijaruhusu wasuluhishi wa mgogoro huo kutoka nje ya nchi hiyo na kusema kuwa serikali ya nchi hiyo itaumaliza mgogoro huo na kusimamia jukumu la ulinzi wa amani katika jimbo la Tigray.

Aidha umoja wa  mataifa umetoa wito kwa serikali ya Ethiopia kuchukua hatua za makusudi na za haraka kutatua mgogoro huo unaoweza kusababisha athari kwa baadhi ya mataifa ya jirani na nchi hiyo.

Mgogoro wa Ethiopia unaripotiwa kusababishwa na hatua ya serikali kuahirisha kufanyika kwa uchaguzi katika jimbo la Tigray uliokuwa umepangwa kufanyika mwaka huu, na kosogezwa mbele hadi mwaka 2021 kutokana na  hofu ya maambukizi ya ugonjwa wa CORONA, hatua ambayo ilipingwa katika jimbo la Tigray iliyopanga kufanya uchaguzi septemba mwaka huu, na kusababisha ghasia kadhaa ambapo  serikali ilitangaza hali ya tahadhari katika jimbo hilo tangu Novemba 4 mwaka huu.