JPM atoa onyo kwa walioteuliwa

0
731

Rais Dkt. John Magufuli ameendelea kuiunda serikali yake ya muhula wa pili ambapo leo amemuapisha Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu, Prof. Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Dkt. Philip Mpango kuwa Waziri wa Fedha na Mipango ikiwa ni hatua za kuendelea kukamilisha baraza la mawaziri.

Akizungumza baada ya kuwaapisha wateule hao, Rais Magufuli amewataka wafanye kazi mara mbili ya walivyokuwa wanafanya katika muhula wa kwanza kwani kipindi hiki hakuna raha na uteuzi wao utategemea na utendaji wao.

Akitolea mfano wa Waziri Mkuu, amesema amona watu mkoani Lindi wakishangilia kuwa wametoa Waziri Mkuu kwa miaka mingine mitano, lakini yeye akasema kazi hiyo haina dhamana kwamba aliyeteuliwa lazima atakaa miaka mitano.

“Kazi ya Uwaziri Mkuu haina guarantee, tategemea na utendaji wake, kwa hiyo tumuombee ili afikie rekodi ya Mhe. Sumaye. Miaka aliyonayo na guarantee ni miaka mitano ambayo ameimaliza, hii mingine ni probability, hivyo tumuombee.”

Amesema kuwa amezunguka nchi nzima na wananchi wamemuamini kwa kumpa kura za kishindo, hivyo kura hizo lazima zionekane katika yale ambayo serikali itayafanya.

“Imani waliyoitoa kwa Chama cha Mapinduzi ni lazima tukaitimize kwa nguvu zote,” amesisitiza Magufuli.

Dkt. Magufuli amesema amelazimika kuanza na wizara hizo mbili kwa sababu masuala ya fedha hayawezi kusubiri hadi ateua baraza zima, na kwamba waziri wa mambo ya nje ni muhimu ili awepo mtu wa kuisemea nchi kimataifa muda wote.