Watatu kizimbani kwa tuhuma za kuchoma moto mabweni ya shule Kilimanjaro

0
286

Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imewafikisha mahakamani washtakiwa watatu wanaohusishwa na matukio ya kuchoma moto bweni la Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Uchira na bweni la Shule ya Sekondari Ebeneza Sango zilizopo wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.


Akizungumza na waandishi wa habari mjini Moshi, Mkurugenzi Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Oswald Tibabyekomya amesema katika tukio la kuchoma moto bweni la shule ya Sekondari ya  Wasichana  Uchira yupo mwalimu mmoja pamoja na mwanafunzi mmoja.


Ameeleza kuwa katika tukio la kuchoma moto bweni la Shule ya sekondari Ebeneza wamemfikisha mahakama mwanafunzi mmoja.


Aidha, amefafanua kuwa, kulingana na upelelezi uliofanyika wamebaini kichocheo kikubwa ni mahusiano mabaya na ushawishi wa vikundi rika visivyofaa shuleni.


Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imesema upelelezi wa matukio hayo pamoja na mengine yanayofanana na haya bado yanaendelea.