Rasmi Dkt. Magufuli aapishwa kwa muhula wa pili

0
367

Dkt. John Magufuli ameapishwa leo katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma kuwa Rais wa Tanzania kwa muhula wa pili baada ya kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28 mwaka huu kwa kupata kura 12,516,252 sawa na asilimia 84.4.

Hafla hiyo ambayo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa inaendelea jijini Dodoma na ilianza kwa Dkt. Magufuli kukagua gwaride la Omega ambapo linaashiria kufikia mwisho wa muhula wake wa kwanza ulioanza 2015.

Baada ya kula kiapo pamoja na mgombea mwenza, Samia Suluhu Hassan, Dkt. Magufuli amekagua gwaride la Alpha ambalo ni ishara ya kuanza muhula wake wa pili utakaomalizika 2025.

Hii ni mara ya kwanza kwa sherehe hizo za kitaifa kufanyika Dodoma, ambapo awali sherehe zote zilikuwa zinafanyika jijini Dar esSalaam. Kufanyika kwa sherehe hizo Dodoma ni jitihada za Rais Dkt. Magufuli za kuihamishia serikali Dodoma.