Rekodi ya haki za binadamu Saudi Arabia kupitiwa

0
1818

Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinakutana mjini Geneva nchini Uswisi kupitia rekodi ya haki za binadamu ya Saudi Arabia katika kipindi hiki ambapo taifa hilo linakabiliwa na shutuma juu ya mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi.

Mkutano huo unaofanyika chini ya Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu ukiwa umepita takribani mwezi mmoja tangu mwandishi huyo wa habari ambaye alikua ni mkosoaji wa ufalme wa Saudi Arabia kuuawa katika ubalozi mdogo wa Saudia Arabia mjini Istanbul nchini Uturuki.

Mkutano huo ambao unawakutanisha wawakilishi kutoka nchi zote 193 Wanachama wa Umoja wa Mataifa, pia unajadili wajibu wa Saudi Arabia kwenye vita vya Yemen, nchi ambayo mwaka 2015 pamoja na washirika wake waliingilia kijeshi vita hiyo ili kumuunga mkono Rais Abedrabbo Mansour Hadi baada ya waasi wanaoungwa mkono na Iran kuchukua udhibiti wa mji mkuu wa Sanaa.

Ujumbe wa Saudi Arabia katika mkutano huo unaongozwa na Bandar Al Aiban ambaye ni mkuu wa Tume ya Haki za Binadamu ya nchi hiyo, ujumbe ambao utawasilisha ripoti ya namna nchi hiyo inavyojitahidi kuheshimu haki za binadamu za kimataifa na pia utajibu maswali na maoni kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu rekodi yao.

Tayari Uingereza, Austria na Uswisi zimewasilisha orodha ya maswali yatakayoulizwa kwenye mkutano huo kuhusu mauaji ya Khashoggi yaliyotokea Oktoba pili mwaka huu.
Saudi Arabia ina rekodi ya kuendelea kutumia adhabu ya kifo, kuwa na ongezeko la adhabu ya kunyonga pamoja na matumizi ya sheria ya kupambana na ugaidi inayolalamikiwa kuwa inatumika vibaya.