Rais Magufuli ashuhudia uzinduzi wa msikiti Chamwino

0
647

Rais Dkt. John Magufuli ameshuhudia uzinduzi wa Msikiti wa Sheikh Abubakar Zubeir Ally uliojengwa Chamwino mkoani Dodoma kwa gharama ya shilingi milioni 319.3 zilizotokana na michango ya viongozi, taasisi na watu mbalimbali.

Ujenzi wa Msikiti huo ulianza tarehe 28 Agosti, 2020 ikiwa ni siku 3 baada ya Rais Magufuli kuitisha harambee ya kuchangisha fedha za kujenga msikiti mpya kwa ajili ya Waislamu wa Chamwino, akiwa katika ibada ya uzinduzi wa Kanisa Katoliki la Bikira Maria Imakulata Ikulu-Chamwino ambalo pia limejengwa kwa harambee aliyoiendeshwa.

Uzinduzi wa msikiti huo umefanywa na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir Ally.

Mkuu wa JKT Mej. Jen. Charles Mbuge amemshukuru Rais Magufuli kwa kuiamini JKT kujenga miradi mbalimbali na amesema kutokana na msikiti huo kujengwa na JKT gharama za ujenzi zimekuwa shilingi milioni 319.3 ikilinganishwa na shilingi Milioni 439.4 kama ujenzi ungefanywa na kampuni za ukandarasi.

Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir Ally amemshukuru Rais Magufuli kwa moyo wake wa upendo na ucha Mungu wake uliomuongoza kuchangisha fedha zilizofanikisha kujengwa kwa msikiti huo, pamoja na msikiti mkubwa wa kimataifa uliojengwa Kinondoni jijini Dar es Salaam ambapo Rais Magufuli alimuomba Mfalme Mohammed VI wa Morocco kufadhili ujenzi huo.

Akizungumza na wananchi waliojitokeza katika sherehe za uzinduzi wa Msikiti huo, Rais Magufuli amemshukuru Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania kwa kukubali harambee ya kuchangia ujenzi wa Msikiti huo, amezishukuru taasisi na watu mbalimbali waliojitokeza kumuunga mkono kuchangia fedha kwa ajili ya ujenzi huo na ameipongeza JKT na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kujenga msikiti mzuri, imara na kwa muda mfupi.

Amesisitiza kuwa baada ya kukamilisha ujenzi huo anadhamiria kufanya harambee nyingine ya kuchangisha fedha kwa ajili dhehebu la dini linalofanya Ibada ya Juma siku ya Jumamosi na ameeleza kuwa atafurahi kuona Ikulu ya Chamwino ikiwa imezungukwa na makanisa na misikiti.