Mazungumzo ya simu kuhusu Kashoggi yanaswa

0
2296

Baadhi ya majarida nchini Marekani yameandika habari inayosema kuwa Mwana wa mfalme wa Saudi Arabia, – Mohammed bin Salman aliwahi kuiambia Marekani kuwa mwandishi wa habari wa Saudi Arabia aliyeuawa Jamal Khashoggi ni mwanachama wa kikundi kimoja cha Kiislam.
Majarida hayo ya Washington Post and New York Times yamedai kuwa Salman alitoa kauli hiyo kwa njia ya simu alipozungumza na maafisa wa Ikulu ya Marekani Oktoba Tisa mwaka huu ikiwa ni wiki moja tangu kutoweka kwa Khashoggi.
Kwa mujibu wa majarida hayo, kauli ya Mwana wa mfalme huyo wa Saudi Arabia aliitoa kabla nchi hiyo haijakiri kuwa mwandishi huyo wa habari aliuawa ndani ya ubalozi mdogo wa nchi hiyo huko Istanbul,- Uturuki.
Katika mazungumzo hayo Salman alieleza kuwa Kashoggi alikua mwanachama wa kikundi cha Muslim Brotherhood na kuiomba Marekani kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili.
Kufuatia kutolewa kwa taarifa za mazungumzo hayo ambayo yalifanyika kwa njia ya simu, familia ya mwandishi huyo wa habari nayo imetoa tamko na kusema kuwa Kashoggi hakuwa mwanachama wa Muslim Brotherhood na kwamba katika uhai wake aliwahi kukanusha jambo hilo mara kadhaa katika miaka ya hivi karibuni.
Habari zaidi zinasema kuwa kauli ya Mwana wa mfalme huyo wa Saudi Arabia inatofautiana na ile aliyoitoa mara baada tu ya mauaji hayo, ambapo alisema kuwa Kashoggi amekufa kifo cha kusikitisha na kwamba nchi hiyo itafanya kila iwezalo kuwatia hatiani wale wote waliohusika na tukio hilo.
Kashoggi aliyefahamika kama mkosoaji wa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia, anadaiwa kuuawa oktoba pili mwaka huu na mwili wake haujpatikana hadi hivi sasa.