Khan ashutumu maandamano Pakistan

0
1791

Waziri Mkuu wa Pakistan, – Imran Khan ameshutumu maandamano yanayoendelea nchini humo kwa mwamvuli wa dini ya kiislamu, yanayopinga hatua ya mahakama nchini humo kubatilisha hukumu ya kifo dhidi ya mwanamke mmoja.

Khan amesema kuwa serikali yake haitaruhusu ghasia zenye mwamvuli wa dini kuondoa amani nchini humo, kwani wananchi wanapaswa kuheshimu vyombo ya dola ikiwemo mahakama.

Kumekuwa na maandamano makubwa ya vitisho nchini Pakistan, baada ya mahakama kuu nchini humo kubatilisha hukumu ya kifo dhidi ya mwanamke huyo Asia Bibi kutoka dini ya kikristo aliyekuwa ametiwa hatiani kwa kosa la kukufuru dini ya kiislam.

Khan amesema kuwa waandamanaji hao hawawakilishi uislamu, bali hisia zao na amewataka wananchi kudumisha amani na kujiepusha katika mikusanyiko isiyofaa, kwa kuwa serikali haitaendelea kuwavumilia.

Mwanamke huyo ambaye ni mama mwenye watoto wanne, alipatikana na hatia baada ya kuchota maji ya kunywa katika chombo chake na kuwapatia wanawake wa kiislamu ili wanywe maji hayo.

Wanawake hao walikasirishwa na hatua hiyo na kudai kuwa Asia amemkufuru mtume, kwani hakupaswa kuwapatia maji akitumia chombo chake.

Asia alitiwa mbaroni miaka minane iliyopita, baada ya wanawake hao kutaka ahukumiwe kifo.