Watumishi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania washitakiwa kwa uhujumu uchumi

0
578

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani imewafikisha watu wanne katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma wakiwemo watumishi watatu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) waliokuwa wakifanya kazi katika kituo cha Kigoma.

Watuhumiwa wamesomewa mashitaka 26 yanayohusiana na uhujumu uchumi na kuisababishia serikali ukosefu wa mapato ya zaidi ya shilingi milioni 600.

Watuhumiwa waliofikishwa mahakamani ni pamoja na Moris Charles, Eliya Stephano Herman Ndiboto na Lusubilo Asisye, huku TAKUKURU ikimtafuta mtuhumiwa Madaraka Robert ambaye mpaka sasa hajulikani alipo. Mamlaka hiyo imewaomba wananchi wanaofahamu alipo kutoa taarifa ili aunganishwe na wenzake katika kesi inayowakabili.


Madaraka Robert

Kaimu Kamanda wa TAKUKURU mkoani Kigoma, Nestor Gatahwa amesema watuhumiwa hao wamehusika na ukwepaji wa kodi, ubadhirifu na utakatishaji fedha uliosababishia mamlaka ya bandari hasara ya shilingi milioni 619.3.

Watuhumiwa wote hawakutakiwa kujibu chochote kutokana mahakama hiyo kutokuwa na kibali cha kusikiliza mashauri hayo, na wamerudishwa mahabusu hadi Oktoba 26 kesi hiyo itakaposikilizwa tena, kutokana na mashitaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana.

Hii ni mara ya pili katika kipindi cha miezi miwili kwa TAKUKURU kuwafikisha makamani watumishi wa mamlaka ya bandari mkoani Kigoma kwa hujuma za ubadhirifu na kusababishia hasara mamlaka hiyo ambapo Septemba 2020 watu watano walifikishwa mahakamani kwa hujuma ya ubadhirifu wa shilingi milioni 153.5.