Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imewataka wanafunzi 28,501 waliodahiliwa zaidi ya Chuo Kikuu kimoja kwa mwaka wa masomo 2020/21, kuthibitisha udahihili wao katika chuo kimoja, ili kuacha nafasi kwa wadahiliwa wengine.
Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa amesema jumla ya waombaji 60,621 walioomba kujiunga na vyuo vikuu mwaka huu, wamefanikiwa kupata udahili huo, licha ya kuwepo wale waliochaguliwa kwenye zaidi ya chuo kimoja.
Katika hatua nyingine, Profesa Kihampa amesema awamu ya pili ya udahili wa shahada ya kwanza kwa mwaka wa masomo 2020/21 itaanza rasmi Oktoba 12 hadi Oktoba 18 mwaka huu.
Moja ya vyuo vikuu vilivyoathiriwa na wanafunzi kudahiliwa mara mbili ni chuo kikuu cha Dar es salaam, ambapo zaidi ya wanafunzi 10,000 wamechaguliwa kujiunga na chuo hicho huku wakiwa pia wamechaguliwa kwenye vyuo vikuu vingine.
Mkurugenzi wa Shahada za awali UDSM Profesa Boniphace Nelson amewataka wanafunzi hao kuthibitisha haraka iwapo wanataka kujiunga na chuo hicho au la.
Kwa mujibu wa TCU, wanafunzi waliochaguliwa kwenye zaidi ya chuo kimoja wamepewa muda wa siku nane hadi Oktoba 17 mwaka huu, kuthibitisha chuo kimoja ambacho wangependa kujiunga na kuacha nafasi kwa waombaji wengine.