Lukuvi: Hakuna kiongozi aliyepora ardhi

0
504

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amekanusha vikali kauli iliyotolewa na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kuwa kuna baadhi ya viongozi wamepora ardhi ikiwemo ardhi ya eneo la Mbarari mkoa wa Mbeya na kusisitiza kuwa hakuna hata kiongozi mmoja aliyepora ardhi.

Lukuvi amesema umilikishaji ardhi nchini unafuata sheria na serikali haina ubaguzi katika kumilikisha mtu yeyoye ardhi huku akiweka wazi kuwa umilikishaji ardhi kwa mtu yeyote hauna kikomo.

“Serikali ya awamu ya tano haina ubaguzi wa kumilikisha ardhi na mwananchi yeyote bila kujali itikadi ya chama cha siasa anaweza kumilikishwa,” amefafanua Lukuvi.

Ameongeza kuwa serikali imechukua hatua mbalimbali kushughulikia masuala ya ardhi ikiwemo kuvibakisha vijiji 920 kati ya 975 vilivyokuwa kwenye hifadhi na kubainisha kuwa, serikali inaangalia namna ya kuvibakisha vijiji vingine 55 vilivyosalia.

Akitolea ufafanuzi suala la Mbarari, Lukuvi alisema wananchi wanaoishi katika vijiji 29 eneo la Mbarari wameamuriwa kubaki eneo hilo ingawa kwa mujibu wa GN Namba 28 ya mwaka 2008 walitakiwa kuondoka lakini kwa huruma ya Rais John Pombe Magufuli alibatilisha uamuzi huo na kuagiza vijiji visiondolewe.

Ameongeza kuwa serikali katika kuwajali wananchi imeamua pia kufuta mapori tengefu 12 yenye zaidi ya hekta 707,659.4 sambamba na kumega hifadhi 14 za misitu kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji.