SGR kuokoa muda unaopotea barabarani

0
586

Ujenzi wa reli ya ya kisasa (SGR) nchini unalenga kuleta maendeleo ya watu kwa kurahisisha muda wa usafiri wa abiria na usafirishaji wa mizigo hatua itakayopunguza muda mwingi unaopotea barabarani na kuwafanya wananchi kuwahi kufanyakazi nyingine za maendeleo.

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi amesema hayo na kuongeza kuwa wizara hiyo itaendelea kuutangaza sana na kuukiulinda mradi huu ili kuwaonesha watanzania nini kinaendelea.

Dkt. Abbasi amesema kuwa Tanzania ipo makini kuwekeza kwenye mambo ambayo ni muhimu katika kuleta manufaa na maendeleo ya watu na kusisitiza kuwa ni utamaduni mpya kwenye nchi yetu kuwa na taifa la wachapakazi, kuwa Watanzania wanaojiamini na kuwa watu wanaopenda mambo mazuri ambayo yanaletwa na Serikali kwa manufaa ya wananchi wake.

“Tunaposema huu ujenzi wa reli ni kitu, ndiyo ni kitu, reli ya SGR ni kitu kinachokwenda kuleta maendeleo ya watu,” amesisitiza Dkt. Abbasi.

Ujenzi wa mradi huo unaendelea ambapo kipande cha Morogoro hadi Mkutupora, Singida kina jumla ya 422km ambapo 336km zinajumuisha njia kuu na 86km sehemu za kupishania treni.