Maonesho wiki ya viwanda yafunguliwa Pwani

0
2012

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ameushauri uongozi wa mkoa wa Pwani kuwaomba wawekezaji mkoani humo kukifanyia marekebisho Chuo cha Ufundi cha mkoa huo ili kitumike kuwafundisha vijana mambo mbalimbali yatakayowawezesha kuajiriwa katika viwanda vilivyopo katika mkoa huo.

Makamu wa Rais ametoa wito huo wilayani Kibaha wakati akifungua maonesho wiki ya viwanda kwa mkoa wa Pwani na kutahadharisha kuwa endapo vijana hao hawatapata elimu, fursa za ajira mkoani humo zitachukuliwa na vijana kutoka mikoa ya jirani.

Pia amezitaka taasisi zinazohusika na maslahi ya wafanyakazi kutembelea maeneo ya viwandani ili kuona namna maslahi ya wafanyakazi hao yanavyoshughulikiwa.

Maonesho hayo ya viwanda mkoani Pwani yanayofanyika katika viwanja vya Sabasaba, yana lengo la kutoa fursa za masoko na kutangaza bidhaa za wajasiriamali wa mkoa huo.

Akiwa katika viwanja hivyo, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na mambo mengine ametembelea mabanda ya kampuni mbalimbali ili kujionea bidhaa zinazotengenezwa hapa nchini.

Awali akimkaribisha Makamu wa Rais kufungua maonesho hayo, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, – Charles Mwijage amesema kuwa serikali inajenga uchumi wa kitaifa na lengo ni kufikia pato la dola elfu tatu za kimarekani kwa mwananchi ifikapo mwaka 2025.

Maonesho ya wiki ya viwanda mkoani Pwani yana kauli mbiu inayosema kuwa Viwanda vyetu, Uchumi wetu, Kwani tumeweza, Tunatekeleza na Tunakuza uchumi wa viwanda.