Visiwa vya Pemba na Unguja kuunganishwa na Mkongo wa Taifa

0
236

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimesaini mkataba wa makubaliano ya kuunganisha visiwa vya Pemba na Unguja na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

Utiaji saini huo umefanywa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Waziri Kindamba kwa upande wa Bara na Mhandisi Shukuru Awadh Suleiman, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Miundombinu ya Tehama Zanzibar (ZICTIA) kwa upande wa Zanzibar.

Kabla ya kushuhudia tukio hilo Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Zainabu Chaula amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejenga Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 700 na kuunganisha kwenye mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na kwenye nchi jirani za Congo, Zambia, Rwanda, Burundi, Kenya, Uganda na Malawi ambapo maunganisho haya yanaenda kufungua fursa za wawekezaji na watumiaji wa huduma za mawasiliano wa ndani na nje ya nchi..
katika kipindi cha miaka mitano tumeshuhudia mifumo ya TEHAMA ambayo inawezesha utoaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi kwa kasi zaidi

Naye Dkt. Mustafa Aboud Jumbe, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar amesema kuwa haya ndio matunda ya mapinduzi yanayopatikana katika nchi yetu, na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetumia zaidi ya shilingi bilioni 30 kuunganisha mikoa na wilaya zote za Unguja na Pemba licha ya changamoto zilizokuwepo katika kuunfanisha mawasiliano ila sasa kwa kupitia makubaliano haya, itatumika njia ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kuunganisha visiwa Pemba na Unguja na hivyo Zanzibar kuunganishwa na Tanzania Bara moja kwa moja na utawezesha kupunguza gharama za mawasiliano.

Ndugu Kindamba amesema kuwa ufunguzi wa njia za mawasiliano ya Mkongo kati ya Tanzania Bara na Zanzibar utakuwa na manufaa makubwa kwa taifa hasa katika kuwezesha kuongezeka kwa matumizi ya takwimu na intaneti na makubaliano hayo yanahusisha kutunza vifaa vya miundombinu ya Tehama vya Zictia kwenye majengo ya TTCL.