Serikali yaeleza sababu ya vyombo vya habari vya kimataifa kuomba leseni

0
216

Serikali imefafanua hatua yake ya kuvitaka vyombo vya habari vya kimataifa vinavyotaka kuvitumia vyombo vya habari vya Tanzania kurusha matangazo yake yana lengo la kutambua vyombo hivyo vinashirikiana vyombo gani vya hapa nchini na sio kuvizuia kutangaza na kuendesha vipindi vyake hapa nchini kama inavyoripotiwa.

Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi Mteule wa Uingereza hapa nchini, Dkt. David Concar na kufafanua kuwa mpaka sasa vyombo vyote vya habari vya kimataifa vimekwishatekeleza matakwa hayo ya kisheria na kupata leseni ya kutangaza na kuendesha vipindi vyao.

Kuhusu suala la mabadiliko ya sheria za asasi za kiraia (NGOs) na vyama vya siasa Prof. kabudi amefafanua kuwa lengo lake lilikuwa ni kuongeza uwazi na uwajibikaji katika fedha zinazoingia kwa asasi hizo pamoja na matumizi yake na kuwa linaendana na sheria na taratibu za kimataifa za kuzuia utakatishaji wa fedha na kuhakikisha makundi yenye nia ovu na misimamo mikali inayokwenda kinyume na tunu za demokrasia hayatumii njia hizo kupenyeza fedha zao.

Dkt. Concar amesema mazungumzo yao mbali na kulenga masuala ya kidiplomasia na maendeleo pia yalilenga kuangalia namna ya kuondoa malalamiko kutoka kwa baadhi ya NGOs na vyombo vya habari vya kimataifa kuhusu kile kinachodaiwa kuwa ni uminywaji wa haki ya uhuru wa vyombo vya habari.

Katika tukio jingine, Prof. Kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Denmark hapa nchini, Mette Norgaard ambapo mbali na suala la uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 hapa nchini, wamejadili pia masuala yanayohusu mashirikiano katika sekta za elimu, afya, biashara na uwekezaji.