Masoko 28 ya madini nchini yaongeza maslahi ya wachimbaji

0
422

Serikali imeanzisha masoko 28 ya madini likiwemo la Nyamongo ili kuwainua wachimbaji wadogo ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya 2015-2020.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema hayo alipokuwa akizungumza na wakazi wa Nyamongo, Nyamwaga na Tarime Mjini, wilayani Tarime, mkoani Mara akimuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Dkt. John Magufuli na wagombea ubunge.

“Kupitia mradi wa usimamizi endelevu wa rasilimali za madini, Serikali imeanzisha masoko 28 ya madini, vituo vidogo 28 vya ununuzi wa madini na ujenzi wa vituo saba vya mafunzo ya umahiri kwa wachimbaji wadogo vya Bariadi, Musoma, Bukoba, Mpanda, Chunya, Songea na Handeni,” amesema.

Ameongeza kuwa mbali na serikali kupata fedha kupitia masoko hayo, pia yamesaidia kupatikana kwa takwimu sahihi za mauzo ya madini, kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata soko la uhakika, kupata bei stahiki kwa bidhaa za madini, kuondoa tatizo la utoroshaji na biashara haramu ya madini.

Akiwafafanulia mambo yaliyofanywa na Serikali ndani ya miaka mitano, Majaliwa amesema baadhi ya kodi kwenye biashara ya madini zenye kero kwa wachimbaji wadogo ikiwemo kodi ya zuio (withholding tax) asilimia tano na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) asilimia 18 zimeondolewa.