Mfanyabiashara ashitakiwa kwa kukwepa kodi milioni 48

0
318

Mfanyabiashara Geofrey Kilimba, mkazi wa Salasala jijini Dar es Salaam, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.

Kilimba amesomewa mashitaka manne ambapo katika shitaka la kwanza, Wakili Mwandamizi wa Serikali Wankyo amedai kuwa, kati ya Agosti 29, 2013 na Agosti 8, 2020 mshitakiwa huyo akiwa na wenzake ambao hawajafikishwa mahakamani, walishirikiana kutenda kosa la uhujumu uchumi nakuongoza genge la uhalifu kunyume na sheria.

Aidha, wakili amedai kuwa katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam mshitakiwa kwa makusudi alikwepa kulipa kodi ya zaidi shilingi milioni 48 ambayo alipaswa kulipa Mamalka ya Mapato Tanzania (TRA).

Katika shitaka la mwisho, Kilimba anadaiwa kati ya Agosti 29, 2013 na Agosti 8,2020 jijini Dar es Salaam , alijipatia kiasi hicho cha fedha huku akijua kuwa fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la kukwepa kulipa kodi TRA.

Hata hivyo mshitakiwa hakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 30, 2020 na mshitakiwa amerudishwa rumande.