Wanne waburuzwa Kisutu kwa tuhuma za uhujumu uchumi

0
382

Watu wanne wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashitaka matatu yakiwemo tuhuma za kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya na utakatishaji fedha.

Akisoma hati ya mashitaka Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi amesema washitakiwa Ernest Michael, Salum Jongo, Amin Sekibo na Tatu Nassor katika tarehe tofauti kati ya Septemba 18, 2020 maeneo ya Vetenari jijini Dar es Salaam walikamatwa wakiwa na 51kg za dawa za kulevya aina ya heroine kinyume na sheria.

Katika shitaka la pili ambalo ni la utakatishaji fedha, washitakiwa hao wanadaiwa kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotokana na biashara haramu ya dawa za kulevya wa zaidi ya shilingi milioni 62 kosa ambalo wanadaiwa kulifanya Septemba 1, 2020 ndani na nje ya nchi.

Aidha, Wakili Kadushi amedai kuwa washitakiwa hao Septemba Mosi mwaka huu jijini Dar es Salaam katika maeneo tofauti walikutwa wakimiliki magari nane ya kifahari, nyumba tatu, laptop moja aina ya Apple na shamba la hekari 19 ambavyo wanadaiwa kujipatia kupitia biashara haramu ya dawa za kulevya.

Hata hivyo wakili huyo amedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo upo katika hatua za mwisho kukamilika hivyo ameomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septamba 30 mwaka huu na washitakiwa wote wamerudishwa rumande.