Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imeondoa zuio la kuingia nchini ililokuwa imeweka kwa Shirika la Ndege la Kenya (KQ) pamoja na kampuni nyingine za usafiri wa anga za nchini humo kwa vipindi tofauti.
Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari ameeleza kuwa mamlaka hiyo imechukua uamuzi huo baada ya Septemba 15, 2020, Kenya kuijumuisha Tanzania katika orodha ya nchi ambazo wageni wake hawatolazimika kuwekwa karantini kwa siku 14 kuthibitika kama hawana maambukizi ya virusi vya corona.
Mbali na KQ, mamlaka hiyo imeondoa zuio kwa kampuni za Fly 540 Limited, Safarilink Aviation na AirKenya Express Limited ambayo ziliwekewa zuio hilo tangu Agosti 25 mwaka huu.
Aidha, Agosti 1, 2020 TCAA ilifuta kibali cha KQ kuingia nchini, uamuzi ambao ulitokana na Kenya kuwataka wageni kutoka Tanzania kukaa karantini kwa siku 14.
TCAA imesema uamuzi wa kuondoa zuio hilo unaanza mara moja na tayari imeitaarifu mamlaka husika nchini Kenya.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza kuwa itaendelea kuheshimu misingi ya makubaliano ya utoaji wa huduma za usafiri wa anga (Chicago Convention 1944 and Bilateral Air Sevice Agreement) kati ya mataifa mawili.