Msaidizi wa Membe hajatekwa, yupo chini ya polisi

0
263

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es salaam, SACP Lazaro Mambosasa, amesema Jerome Luanda ambaye ni msaidizi wa Bernard Membe yuko mikononi mwa polisi na anashangazwa na wanaosema ametekwa na watu wasiojulikana.

Kamanda Mambosasa amesema Luanda anashikiliwa na polisi kwa kosa la utakatishaji fedha.

“Na huyu nasema amekamatwa, anatuhumiwa kwa kosa la kutakatisha fedha, kwahiyo anayetaka kuthibitisha hilo ni suala la kuja tumueleze ukweli wa jambo hilo.”

Kauli hii ya Mambosasa imekuja baada ya taarifa kusambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa msaidizi huyo wa mgombea urais wa Tanzania kupitia ACT-Wazalendo alitekwa baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).