Wakala wa misitu waibuka kidedea mashindano ya biashara

0
285

Wizara ya Maliasili na Utalii na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) wameibuka kidedea kwa kuwa mshindi wa jumla miongoni mwa taasisi za serikali katika maonesho ya biashara ya Afrika Mashariki yanayofanyika jijini Mwanza kwa utoaji wa huduma bora kwa jamii.

Waandaaji wa maonesho hayo, Chama cha Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA), wamewakabidhi kombe la ushindi wizara ya maliasili na TFS kwa kutambua na kuthamini mchango wa wizara na taasisi hiyo katika jamii.

Akizungumza katika maonesho hayo yanayofanyika mara moja kwa mwaka Mkuu wa Kitengo cha Ugani na Uenezi kutoka TFS Kanda ya Ziwa, Pius Mbilla amewashukuru TCCIA kwa kutambua mchango wao katika utoaji wa huduma bora na kuahidi kuendelea kushikamana na jamii katika kukuza uchumi wa taifa.

Baadhi ya wataalamu kutoka TFS licha ya kushukuru kwa kupewa tuzo hiyo wamesema jukumu lao ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ili kuchochea maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.