Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), John Magufuli ameahidi kuwa endapo atashinda, serikali yake utanunua ndege tano mpya ndani ya miaka mitano.
Dkt. Magufuli amesema hayo akiwahutubia maelfu ya wananchi waliokusanyika katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma kwenye uzinduzi wa kampeni za chama hicho ikiwa ni safari ya kuelekea Agosti 28, 2020.
Mgombea huyo amesema kuwa kati ya ndege tano zitakazonunuliwa, ndege mbili zitakuwa ni za masafa marefu, mbili masafa mafupi na moja itakuwa ya kubeba mizigo.
Kwa miaka mitano iliyopita, serikali imenunua ndege 11 lakini hadi sasa zilizopokelewa nchini ni ndege 8. Ndege hizo ni Boeing 787-8 Dreamliner mbili, Airbus 220-300 aircraft mbili na Bombardier Dash 8-400 nne.
Mbali na hilo, amesema serikali yake itaimarisha ukuaji wa uchumi kwa kuwekeza zaidi kwenye sekta mbalimbali zikiwemo utalii, kilimo na uvuvi. Serikali pia itahakikisha ongezeko la ajira na uwepo wa amani ili kuvutia wawekezaji.