Serikali ya Tanzania imepokea mkopo wa masharti nafuu wa dola milioni 4.5 (shilingi bilioni 33.9) kutoka Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait (KFED) kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa umwagiliaji katika Bonde la Mto Luiche mkoani Kigoma.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya fedha na Mipango, Benny Mwaipaja amesema kuwa mkataba huo umesainiwa nchini Kuwait kati ya Balozi wa Tanzania nchini humo, Aisha Amour, kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Mkurugenzi Mkuu wa KFED, Abdulwahad Ahmed Al- Bader, kwa niaba ya Serikali ya Kuwait.
“Fedha hizo za mkopo zitatumika katika uhakiki wa usanifu wa kina wa mradi na usimamizi wa ujenzi wa bwawa la maji la mita 375 lenye uwezo wa kuhifadhi lita za ujazo milioni 70 za maji,” amesema Mwaipaja.
Fedha hizo pia zitatumika katika ujenzi wa miundombinu kama mifereji ya maji, kinga za mafuriko, daraja na barabara zitakazotumika kutoa huduma zenye urefu wa kilometa 21.
Mwaipaja ameongeza kuwa mradi huo unategemewa katika kuongeza wigo wa kilimo cha umwagiliaji kwa takribani eneo la hekta 3,000 na kutoa fursa za ajira mbalimbali kabla na baada ya kuanza kutekelezwa kwa mradi.
Zao ambalo linatarajiwa kuzalishwa katika eneo la mradi ni mpunga, zao hilo linatarajiwa kuongeza kipato cha wakulima lakini pia kutekelezwa kwa dhana ya Serikali ya kuwa na kilimo cha kisasa kitakachoongeza usalama wa chakula nchini.