TBC yatoa tamko kufuatia kufukuzwa kwenye mkutano wa CHADEMA

0
2225

Kufuatia kitendo cha Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe kuamrisha kufukuzwa kwa watumishi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) wakati wanarusha matangazo mbashara ya uzinduzi wa kampeni za chama hicho, TBC imetoa tamko la kulaani hatua hiyo.

TBC imesema kuwa vituo vya TBC1 na TBC Taifa vilikuwa vikirusha matangazo hayo kwa mujibu wa sheria na kanuni za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

“Kitendo cha uongozi wa CHADEMA kutangaza kuwafukuza watangazaji wa TBC si cha kiuungwa na kinahatarisha usalama wa watendaji hao na vifaa vyao,” imeeleza taarifa hiyo.

TBC imesema kuwa mbali na kuwa itatoa taarifa Polisi na NEC, imesitisha kurusha matangazo ya chama hicho hadi hapo watendaji wake watakapohakikishiwa usalama.

“TBC inapenda kutimiza wajibu wake wa kisheria na imekuwa tayari siku zote kufanya kazi na vyama vyote bila ubaguzi,” imehitimisha taarifa ya TBC.

Wakati wa uzinduzi wa kampeni hizo, Mbowe alidai kuwa TBC imekata matangazo hayo, jambo ambalo halikuwa sahihi kwani hadi wakati anatoa taarifa hiyo, matangazo yalikuwa hewani. Kufuatia madai hayo, Mbowe aliwaamrisha watendaji wa TBC kuondoka uwanjani hapo ndani ya dakika 15.