NEC yafungua pazia fomu za wagombea Urais

0
433

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) leo itaanza kutoa fomu kwa wagombea wa Urais na wagombea wenza zoezi litakalokamilia Agosti 25 mwaka huu jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Semistocles Kaijage amesema kuwa wagombea wa nafsi hizo walioteuliwa na vyama vyao vya siasa vyenye usajili wa kudumu, wajitokeze katika kipindi hiki ili kuchukua fomu za kugombea.

Vyama mbalimbali tayari vimeteuwa wagombea wa urais pamoja na wagombea wenza katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.

Chama cha Mapinduzi (CCM) ndicho kilifungua pazi la uteuzi ambapo kimemteua Rais John Magufuli kugombea kwa muhula wa pili, huku mgombea mwenza akiwa ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu.

Kwa upande wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) chenyewe kimemteua Wakili Tundu Lissu kupeperusha bendera ya chama huku akisaidiwa na Salum Mwalimu.

John Shibuda amepitishwa kugombea kupitia Chama cha ADATadea huku Profesa Ibrahim Lipumba atapeperusha bendera ya Chama Cha Wananchi (CUF).

Wakati hayo yakiendelea Chama cha ACT Wazalendo kinatarajia kuteua mgombea wake leo ambapo tayari kada wa chama hicho Bernard Membe ametia nia ya kuomba kuteuliwa kugombea.

Kampeni za Uchaguzi Mkuu zitaanza Agosti 26 mwaka huu na kumalizika Otoba 27 mwaka huu.