Serikali yatoa bilioni 20 kulipa madeni ya korosho

0
469

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imetoa shilingi bilioni 20 za kulipa madeni ya wakulima, wasafirishaji, wapuliziaji dawa na waendesha maghala ya korosho.

Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wanachama wa Chama cha Msingi (AMCOS) cha Matogoro na wakazi wa Tandahimba mkoani Mtwara alipokwonda kuhamasisha maandalizi ya msimu wa ununuzi wa korosho.

“Rais Magufuli ametoa fedha hizi kwa ajili ya Tandahimba, Masasi, Mtwara na Kibiti kwa ajili ya waliokuwa wamelipwa nusu, waliolipwa kiasi na wasiolipwa kabisa. Fedha hizi zitaanza kulipwa kesho [Julai 20] asubuhi,” amesema.

Amesema uhakiki uliofanywa kwa wakulima wa Kibiti, Rufiji, Mkuranga, Ruangwa, Liwale, Lindi, Tunduru na wilaya zote za mkoa wa Mtwara ulibaini kuwa wakulima na watoa huduma wote walikuwa wakidai zaidi ya sh. bilioni 23.

“Katika hao, Tandahimba wanadai zaidi ya shilingi bilioni 9, Masasi wanadai bilioni 2.3 na Mtwara Vijijini wanadai milioni 884. Nyingine ni za Pwani na Lindi,” amefafanua.

Waziri Mkuu amesema fedha hizo zimetokana na mfumo uliotengenezwa na wanunuzi ili kumnyonya mkulima katika msimu wa 2018/2019 kwa kununua kilo ya korosho kwa sh. 1,500 badala ya sh. 3,000 hali iliyolazimu Serikali kuingilia kati na kuamua kuzinunua korosho zote.

Waziri Mkuu alishuhudia Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Kilimo (TABD), Japhet Justine akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa hundi ya shilingi bilioni 9.05 ambaye pia aliikabidhi kwa viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Tandahimba na Newala (TANECU) na AMCOS ya Matogoro.

Awali, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mtwara, Yusuph Nanila alimuomba Waziri Mkuu atoe majibu ya lini wakulima wa Tandahimba watalipwa fedha zao, ambazo zimefikia zaidi ya shilingi bilioni 9.