Waziri Mhagama: Wanawake mgombee msisubiri nafasi za upendeleo

0
224

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amewaasa wanawake kutokubali kutumiwa na vyama vya siasa kama mawakala bali nao wajitokeze kwa wingi kugombea.


Waziri Mhagama ametoa wito jijini Dodoma wakati akizungumza na umoja wa wanawake viongozi wa vyama vya siasa nchini.

Waziri huyo amesema wanawake wana nguvu kubwa na uwezo wa kuwa viongozi ndiyo maana Rais Dk John Magufuli amewaamini katika nafasi mbalimbali na hata wakati alipoteuliwa na chama chake kuwa mgombea Urais wa CCM alimchagua tena Mama Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza wake kwa mara pili.

“Nguvu yetu wanawake ni kubwa sana na kipindi hiki tunapoelekea kwenye uchaguzi nitoe rai kwenu kugombea nafasi za uongozi kupitia vyama vyenu, chukueni fomu mkachuane kwenye majimbo na kata msiogope kwa sababu uwezo tunao.

Tusikubali kusubiri nafasi za upendeleo kama tuna lengo la kufikia 50/50 basi inatulazimu pia tuingie kwenye uwanja wa mapambano ili tupime nguvu zetu, na kwa sababu sisi tuna uwezo mkubwa basi naamini tutashinda,” amesema Mhagama.

Kwa upande wake Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mtungi akizungumzia hoja aliyoitoa Rais kuhusu uchaguzi kuwa huru na wa haki, amesema siyo tu kwamba uchaguzi utakuwa huru na wa haki, bali unapaswa kumalizika kwa Amani.