Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ameziagiza halmashauri zote nchini kusimamia utunzaji wa vyanzo vya maji ili kudhibiti vyanzo hivyo visiharibiwe na watu wanaoendesha shughuli za kibinadamu.
Makamu wa Rais ametoa agizo hilo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wakati akikagua mradi wa upanuzi wa mtambo wa maji wa Ruvu Chini unaofanywa kwa pamoja na ujenzi wa tanki kubwa ambalo litatumika kusambaza maji kwenye mji wa Bagamoyo na vijiji jirani.
Amesema kuwa serikali imetumia gharama kubwa kutekeleza mradi huo ili kuondoa kabisa tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama katika miji ya Bagamoyo na Dar es salaam, hivyo ni vema halmashauri nchini zikaweka utaratibu mzuri wa kutunza vyanzo hivyo.
Akiwa katika wilaya hiyo ya Bagamoyo ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku sita mkoani Pwani, Makamu wa Rais amewaomba Watanzania wote kutunza miundombinu ya maji inayojengwa katika maeno yao.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo amemueleza Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa hali ya upatikanaji wa maji katika mkoa huo imeongezeka hadi kufikia asilimia 51 kwa maeneo ya mijini na asilimia 62 kwa maeneo ya vijijini.